6 Katika mwaka wa kenda wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi.
7 Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya BWANA, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine.
8 Wakaziendea sheria za mataifa, ambao BWANA aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya.
9 Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya BWANA, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma.
10 Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi;
11 wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu, kama mataifa walivyofanya, ambao BWANA aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo mabaya, ili wamkasirishe BWANA;
12 wakatumikia sanamu, ambazo BWANA aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili.