2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Abiya, binti Zekaria.
3 Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, mfano wa yote aliyoyafanya Daudi, baba yake.
4 Alipaondoa mahali pa juu, akazibomoa nguzo, akaikata hiyo Ashera; akaivunja vipande vipande ile nyoka ya shaba aliyoifanya Musa; maana hata siku zile wana wa Israeli walikuwa wakiifukizia uvumba; naye akaiita jina lake Nehushtani.
5 Alimtumaini BWANA, Mungu wa Israeli; hata baada yake hapakuwa na mfano wake katika wafalme wote wa Yuda, wala katika hao waliomtangulia.
6 Maana alishikamana na BWANA, hakuacha kumfuata, bali alizishika amri zake BWANA alizomwamuru Musa.
7 Naye BWANA akawa pamoja naye, kila alikokwenda alifanikiwa; tena alimwasi mfalme wa Ashuru, wala hakumtumikia.
8 Akawapiga Wafilisti mpaka Gaza na mipaka yake, tangu mnara wa walinzi hata mji wenye boma.