30 Wala Hezekia asiwatumainishe katika BWANA, akisema, Hakika BWANA atatuokoa, wala mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.
31 Msimsikilize Hezekia; kwa sababu mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie; mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika lake mwenyewe;
32 hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya chakula na mashamba ya mizabibu, nchi ya mafuta ya mzeituni na asali, ili mpate kuishi, msife; wala msimsikilize Hezekia, awadanganyapo, akisema, BWANA atatuokoa.
33 Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake wakati wo wote na mkono wa mfalme wa Ashuru?
34 Iko wapi miungu ya Hamathi, na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, na ya Hena, na ya Iva? Je! Imeuokoa Samaria na mkono wangu?
35 Katika miungu ya nchi hizi zote, ni miungu gani iliyookoa nchi yao na mkono wangu, hata BWANA auokoe Yerusalemu na mkono wangu?
36 Lakini hao watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana amri ya mfalme ilikuwa kwamba, Msimjibu neno.