1 Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu.
2 Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya BWANA.
3 Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile.
4 Kisha, mfalme akamwamuru Hilkia, kuhani mkuu, na makuhani wa daraja ya pili, na walinzi wa mlango, kwamba watoe katika hekalu la BWANA vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali, na kwa ajili ya Ashera, na kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni; akavipiga moto nje ya Yerusalemu, katika mashamba ya Ridroni, akayachukua majivu yake mpaka Betheli.
5 Akawaondosha wale makuhuni walioabudu sanamu, ambao wafalme wa Yuda waliwaweka ili kufukiza uvumba katika mahali pa juu, ndani ya miji ya Yuda, na katika kila mahali, pande zote za Yerusalemu; na hao pia waliomfukizia uvumba Baali, na jua, na mwezi, na sayari, na jeshi lote la mbinguni.
6 Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya BWANA, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuiponda-ponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu.
7 Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa BWANA, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera.