4 Kisha, mfalme akamwamuru Hilkia, kuhani mkuu, na makuhani wa daraja ya pili, na walinzi wa mlango, kwamba watoe katika hekalu la BWANA vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali, na kwa ajili ya Ashera, na kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni; akavipiga moto nje ya Yerusalemu, katika mashamba ya Ridroni, akayachukua majivu yake mpaka Betheli.
5 Akawaondosha wale makuhuni walioabudu sanamu, ambao wafalme wa Yuda waliwaweka ili kufukiza uvumba katika mahali pa juu, ndani ya miji ya Yuda, na katika kila mahali, pande zote za Yerusalemu; na hao pia waliomfukizia uvumba Baali, na jua, na mwezi, na sayari, na jeshi lote la mbinguni.
6 Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya BWANA, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuiponda-ponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu.
7 Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa BWANA, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera.
8 Akawatoa makuhani wote katika miji ya Yuda, akapanajisi mahali pa juu, makuhani walipokuwa wamefukiza uvumba, tangu Geba hata Beer-sheba; akapavunja mahali pa juu pa malango, palipokuwapo penye kuingia lango la Yoshua, liwali wa mji, palipokuwa upande wa kushoto wa mtu langoni pa mji.
9 Walakini hao makuhani wa mahali pa juu hawakupanda madhabahuni kwa BWANA katika Yerusalemu, bali wakala mikate isiyo na chachu katikati ya ndugu zao.
10 Naye akainajisi Tofethi, iliyomo katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu asipitishe mwana wake au binti yake motoni kwa Moleki.