1 Katika siku zake akakwea Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na Yehoyakimu akawa mtumishi wake muda wa miaka mitatu; kisha, akageuka, akamwasi.
2 Naye BWANA akatuma juu yake vikosi vya Wakaldayo, na vikosi vya Washami, na vikosi vya Wamoabi, na vikosi vya wana wa Amoni, akawatuma juu ya Yuda ili kuiharibu, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa mkono wa watumishi wake manabii.
3 Hakika kwa amri ya BWANA mambo hayo yalimpata Yuda, ili waondoshwe kutoka machoni pake, kwa sababu ya dhambi zake Manase, kadiri ya yote aliyoyafanya;
4 tena kwa ajili ya damu zisizo na hatia alizozimwaga; kwani aliujaza Yerusalemu damu zisizo na hatia; wala BWANA hakukubali kusamehe.
5 Basi mambo yote ya Yehoyakimu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
6 Yehoyakimu akalala na babaze; na mwanawe Yekonia akatawala mahali pake.