1 Basi Yoramu mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na nane wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka kumi na miwili.
2 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA; ila si kama baba yake na kama mama yake; maana akaiondoa ile nguzo ya Baali aliyoifanya baba yake.
3 Pamoja na hayo alishikamana na dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo kwa hizo aliwakosesha Israeli; wala hakuziacha.
4 Basi Mesha, mfalme wa Moabu, alikuwa mfuga kondoo; naye alikuwa akimlipa mfalme wa Israeli sufu ya wana-kondoo elfu mia, na ya kondoo waume elfu mia.
5 Lakini ikawa, Ahabu alipokufa, mfalme wa Moabu akamwasi mfalme wa Israeli.
6 Akatoka wakati ule ule mfalme Yoramu katika Samaria, akawahesabu Israeli wote.