12 Yehoshafati akasema, Neno la BWANA analo huyu. Basi mfalme wa Israeli, na Yehoshafati, na mfalme wa Edomu, wakamshukia.
13 Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, Nina nini mimi nawe? Uende kwa manabii wa babayo, na manabii wa mamayo. Mfalme wa Israeli akamwambia, La, sivyo; kwa kuwa BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu.
14 Elisha akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo, ambaye nimesimama mbele zake, kama singemwangalia uso wake Yehoshafati mfalme wa Yuda, singekutazama, wala kuonana nawe.
15 Ila sasa niletee mpiga kinanda. Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga, mkono wa BWANA ukamjia juu yake.
16 Akasema, BWANA asema hivi, Fanyeni bonde hili lijae mahandaki.
17 Kwa kuwa BWANA asema hivi, Hamutauona upepo, wala hamtaiona mvua, ila bonde hilo litajaa maji; nanyi mtakunywa, ninyi, na ng’ombe zenu, na wanyama wenu.
18 Na jambo hili ni jepesi machoni pa BWANA; pia atawatia Wamoabi mikononi mwenu.