16 Lakini akasema, Kama BWANA aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa.
17 Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa BWANA.
18 Jambo hili BWANA amwachilie mtumwa wako; bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni ili aabudu humo, naye akitegemea mkononi mwangu, nami nikijiinama nyumbani mwa Rimoni, hapo ninapojiinama nyumbani mwa Rimoni, BWANA amwachilie mtumwa wako jambo hili.
19 Akamwambia, Enenda kwa amaniBasi akamwondokea mbali kidogo.
20 Lakini Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama BWANA aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake.
21 Basi Gehazi akamfuata Naamani. Naye Naamani, alipoona mtu apigaye mbio anakuja nyuma yake, alishuka garini amlaki, akasema, Je! Ni amani?
22 Akasema, Amani. Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana na manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili.