1 Nabii Elisha akamwita mmojawapo wa wana wa manabii, akamwambia, Jikaze viuno, ukachukue chupa hii ya mafuta mkononi mwako, ukaende Ramoth-Gileadi.
2 Utakapofika huko, mtafute Yehu, mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, ukaingie, ukamtoe miongoni mwa ndugu zake, ukamchukue katika chumba cha ndani.
3 Kisha, ukatwae ile chupa ya mafuta, ukayamimine juu ya kichwa chake, ukaseme, BWANA asema hivi, Nimekutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli. Kisha ufungue mlango ukakimbie, wala usikawie.
4 Basi yule kijana, yule nabii kijana, akaenda Ramoth-Gileadi.
5 Naye alipofika, tazama, majemadari wa jeshi walikuwa wamekaa; naye akasema, Nimetumwa na neno kwako, Ee jemadari; Yehu akasema, Kwa yupi miongoni mwetu sote? Akasema, Kwako wewe, Ee jemadari.