13 Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana,
14 akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, nami nitawaongezea; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge.
15 Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Mungu, ili alithibitishe neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa mkono wa Ahiya Mshiloni.
16 Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hawasikilizi, watu wakamjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli, kila mtu; sasa itunze nyumba yako mwenyewe, Daudi. Basi wakaenda zao Israeli wote hemani kwao.
17 Lakini kwa habari za wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu alitawala juu yao.
18 Ndipo mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, msimamizi wa shokoa; nao wana wa Israeli wakamtupia mawe, hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda garini mwake, ili akimbilie Yerusalemu.
19 Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi, hata leo.