1 Ndipo roho ya Mungu ikamjia Azaria mwana wa Odedi;
2 naye akatoka ili amlaki Asa, akamwambia, Nisikieni, Ee Asa, na Yuda wote na Benyamini; BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.
3 Basi tangu siku nyingi Israeli wamekuwa hawana Mungu wa kweli, wala hawana kuhani afundishaye, wala hawana torati;
4 lakini walipomgeukia BWANA, Mungu wa Israeli, katika msiba wao, na kumtafuta, akaonekana kwao.
5 Hata na zamani zile hakukuwa na amani kwake atokaye, wala kwake aingiaye, ila fadhaa kubwa juu yao wote wakaao katika nchi.
6 Wakavunjika-vunjika, taifa juu ya taifa, na mji juu ya mji; kwani Mungu aliwafadhaisha kwa shida zote.
7 Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na ijara.