1 Basi Sulemani alikusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, na kuujengea ufalme wake nyumba.
2 Sulemani akahesabu watu sabini elfu wawe wachukuzi wa mizigo, na watu themanini elfu wawe wachongaji milimani, na elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao.
3 Sulemani akatuma watu kwa Hiramu mfalme wa Tiro, akisema, Kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, na kumletea mierezi, ajijengee nyumba ya kukaa, unitendee na mimi.
4 Angalia, najenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, ili kumfanyia wakfu, ya kufukizia mbele zake fukizo la manukato, na ya mkate wa wonyesho wa daima, na ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na za siku za sabato, na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoagizwa za BWANA, Mungu wetu. Hili ni agizo la milele kwa Israeli.