1 Nao wenyeji wa Yerusalemu walimfanya Ahazia mwanawe mdogo awe mfalme mahali pake; maana wakubwa wote wamekwisha kuuawa na kikosi cha watu waliokuja matuoni pamoja na Waarabu. Hivyo akatawala Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda.
2 Ahazia alikuwa na umri wa miaka arobaini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Athalia binti Omri.
3 Yeye naye akaziendea njia za nyumba ya Ahabu; kwa kuwa mamaye alikuwa mshauri wake katika kufanya maovu.
4 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kama nyumba ya Ahabu; kwa kuwa hao walikuwa washauri wake, alipokwisha kufa babaye, hata aangamie.