7 Kwa kuwa wana wa Athalia, yule mwanamke mwovu, walikuwa wameibomoa nyumba ya Mungu; na vitakatifu vyote vya nyumba ya BWANA wamewapatia mabaali.
8 Basi mfalme akaamuru, nao wakafanyiza kasha, wakaliweka nje langoni pa nyumba ya BWANA.
9 Wakapiga mbiu katika Yuda na Yerusalemu, kumletea BWANA kodi aliyoiweka Musa mtumishi wa Mungu, juu ya Israeli jangwani.
10 Wakafurahi maakida wote na watu wote, wakaleta na kutia ndani ya kasha, hata wakaisha.
11 Ikawa wakati walipoletewa kasha wasimamizi wa mfalme kwa mkono wa Walawi, nao wakaona ya kwamba kuna fedha nyingi, huja karani wa mfalme, na msimamizi wake kuhani mkuu, wakatoa yaliyomo kashani, kisha hulichukua kasha, na kulirudisha mahali pake. Ndivyo walivyofanya siku kwa siku, wakakusanya fedha tele.
12 Na mfalme na Yehoyada waliwapa hao waliofanya kazi ya utumishi wa nyumba ya BWANA; nao wakawaajiri waashi na maseremala ili kuitengeza nyumba ya BWANA, na hao pia wafuao chuma na shaba ili kuitengeza nyumba ya BWANA.
13 Hivyo mafundi wakafanya kazi yao, nao wakaimaliza, wakaisimamisha nyumba ya Mungu kama ilivyopasa, wakaifanya imara.