1 Hezekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka ishirini na kenda; na jina la mamaye aliitwa Abiya binti Zekaria.
2 Akafanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Daudi babaye.
3 Yeye, katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, katika mwezi wa kwanza, aliifungua milango ya nyumba ya BWANA, akaitengeneza.
4 Akawaingiza makuhani na Walawi, akawakusanya uwandani upande wa mashariki,
5 akawaambia, Nisikieni, enyi Walawi; jitakaseni nafsi zenu sasa, mkaitakase na nyumba ya BWANA, Mungu wa baba zenu, mkautoe uchafu katika patakatifu.
6 Kwa maana baba zetu wameasi, na kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, Mungu wetu, wamemwacha, na kugeuzia mbali nyuso zao na makao ya BWANA, na kumpa maungo.