2 Akafanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Daudi babaye.
3 Yeye, katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, katika mwezi wa kwanza, aliifungua milango ya nyumba ya BWANA, akaitengeneza.
4 Akawaingiza makuhani na Walawi, akawakusanya uwandani upande wa mashariki,
5 akawaambia, Nisikieni, enyi Walawi; jitakaseni nafsi zenu sasa, mkaitakase na nyumba ya BWANA, Mungu wa baba zenu, mkautoe uchafu katika patakatifu.
6 Kwa maana baba zetu wameasi, na kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, Mungu wetu, wamemwacha, na kugeuzia mbali nyuso zao na makao ya BWANA, na kumpa maungo.
7 Tena wameifunga milango ya ukumbi, na kuzizima taa, wala hawakufukiza uvumba, wala hawakumtolea Mungu wa Israeli sadaka za kuteketezwa katika patakatifu.
8 Kwa hiyo hasira ya BWANA imekuwa juu ya Yuda na Yerusalemu, naye amewatoa kuwa matetemeko, wawe ushangao, na mazomeo, kama mwonavyo kwa macho yenu.