1 Ndipo Sulemani akaanza kuijenga nyumba ya BWANA huko Yerusalemu, juu ya mlima Moria, pale BWANA alipomtokea Daudi babaye alipotengeza mahali pale alipoagiza Daudi, katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi.
2 Akaanza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa kutawala kwake.
3 Basi hii ndiyo misingi ya majengo ya nyumba ya Mungu aliyoiweka Sulemani. Urefu wake kwa mikono ya cheo cha kwanza ulikuwa mikono sitini, na upana wake mikono ishirini.
4 Na ukumbi uliokuwa mbele yake, urefu wake kadiri ya upana wa nyumba ulikuwa mikono ishirini, na kwenda juu kwake mia na ishirini; akaufunikiza ndani kwa dhahabu safi.