8 Hata walipokuja Hezekia na wakuu, na kuziona zile chungu, wakamhimidi BWANA, na watu wake Israeli.
9 Ndipo Hezekia akaulizana na makuhani na Walawi katika habari ya hizo chungu.
10 Azaria kuhani mkuu, wa nyumba ya Sadoki, akamjibu, akasema, Tangu watu walipoanza kuleta matoleo nyumbani kwa BWANA, tumekula na kushiba, na kusaza tele; kwa kuwa BWANA amewabariki watu wake; na kilichosalia ndiyo akiba hii kubwa.
11 Ndipo Hezekia akaamuru kutengeneza vyumba nyumbani mwa BWANA; wakavitengeneza.
12 Wakayaingiza matoleo na zaka na vitu vilivyowekwa wakfu, kwa uaminifu; na juu yake Konania Mlawi alikuwa mkuu, na wa pili ni Shimei nduguye.
13 Na Yehieli, na Azaria, na Nahathi, na Asaheli, na Yerimothi, na Yozabadi, na Elieli, na Ismakia, na Mahathi, na Benaya, walikuwa wasimamizi chini ya mkono wa Konania na Shimei nduguye, kwa amri ya Hezekia mfalme, na Azaria mkuu wa nyumba ya Mungu.
14 Na Kore, mwana wa Imna, Mlawi, bawabu wa mlango wa mashariki, alizisimamia sadaka za hiari za Mungu; ili kugawa matoleo ya BWANA, navyo vitu vilivyokuwa vitakatifu sana.