1 Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu.
2 Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaziendea njia za Daudi babaye, asigeuke kwa kuume wala kwa kushoto.
3 Kwa kuwa katika mwaka wa nane wa kutawala kwake, naye akali mchanga, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi babaye; hata katika mwaka wa kumi na mbili akaanza kusafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuondoa mahali pa juu, na kwa kuondoa maashera, na sanamu za kuchora, nazo za kusubu.
4 Wakazibomoa madhabahu za mabaali machoni pake; na sanamu za jua, zilizoinuliwa juu yake, akazikata-kata; na maashera, na sanamu za kuchonga, nazo za kusubu, akazivunja-vunja, akaziponda kuwa mavumbi, akayamimina juu ya makaburi ya hao waliozichinjia dhabihu.