12 Nao watu wakatenda kazi kwa uaminifu; na wasimamizi wao walikuwa Yahathi na Obadia, Walawi, wa wana wa Merari; na Zekaria na Meshulamu, wa wana wa Wakohathi, ili kuihimiza kazi; na wengine katika Walawi, wote waliokuwa wastadi wa kupiga vinanda.
13 Tena walikuwa juu ya wachukuzi wa mizigo, wakawahimiza wote waliotenda kazi ya huduma yo yote; na miongoni mwa Walawi kulikuwa na waandishi, na wasimamizi, na mabawabu.
14 Nao walipotoa ile fedha iliyoletwa nyumbani mwa BWANA, Hilkia kuhani akakiona kitabu cha torati ya BWANA iliyotolewa kwa mkono wa Musa.
15 Akajibu Hilkia akamwambia Shafani mwandishi, Kitabu cha torati nimekiona nyumbani mwa BWANA. Hilkia akampa Shafani kile kitabu.
16 Shafani akampelekea mfalme hicho kitabu, tena akampasha mfalme habari, akisema, Yote waliyokabidhiwa watumishi wako, wayafanya.
17 Nao wameimimina fedha iliyoonekana nyumbani mwa BWANA, nayo wameitia mikononi mwa wasimamizi, na mikononi mwa watenda kazi.
18 Shafani mwandishi akamweleza mfalme, akisema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akasoma ndani yake mbele ya mfalme.