1 Watu wa nchi wakamtwaa Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtawaza awe mfalme katika Yerusalemu badala ya babaye.
2 Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu.
3 Naye mfalme wa Misri akamwondoa katika Yerusalemu, akaitoza nchi talanta mia za fedha, na talanta moja ya dhahabu.
4 Mfalme wa Misri akamtawaza Eliakimu nduguye awe mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu, akambadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu. Neko akamtwaa Yehoahazi nduguye, akamchukua mpaka Misri.
5 Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja; akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, Mungu wake.
6 Juu yake akakwea Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akamfunga kwa pingu, amchukue mpaka Babeli.
7 Nebukadreza akachukua baadhi ya vyombo vya nyumba ya BWANA mpaka Babeli, akavitia katika hekalu lake huko Babeli.