1 Tena akafanya madhabahu ya shaba, mikono ishirini urefu wake, na mikono ishirini upana wake, na mikono kumi kwenda juu kwake.
2 Tena akaifanya bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ya mviringo, na kwenda juu kwake ilikuwa mikono mitano; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa.
3 Na chini yake palikuwa na mifano ya ng’ombe, walioizunguka pande zote, kwa mikono kumi, wakiizunguka pande zote ile bahari. Ng’ombe walikuwa safu mbili, wakayeyushwa hapo ilipoyeyushwa hiyo bahari.
4 Ikakaa juu ya ng’ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani.
5 Na unene wake ulikuwa nyanda nne, na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu tatu, kukaa ndani yake.
6 Akafanya na birika kumi, akaziweka tano upande wa kuume, na tano upande wa kushoto, za kuoshea; ndizo walizooshea mambo ya kafara; lakini hiyo bahari ilikuwa ya makuhani ya kuogea.