20 Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani.
21 Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu zilizokwenda Tarshishi pamoja na watumishi wa Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi.
22 Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima.
23 Wafalme wote wa duniani wakamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni.
24 Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka.
25 Sulemani akawa na mazizi ya farasi na magari elfu nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.
26 Akatawala juu ya wafalme wote toka Mto hata nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri.