20 Kwa kuwa umekuja jana tu kwa nini nikusumbue leo, na kukuzungusha huko na huko pamoja nasi nami hapa naenda niwezapo kwenda? Rudi wewe, ukawarudishe na ndugu zako; rehema na kweli ziwe pamoja nawe.
21 Naye Itai akamjibu mfalme akasema, Kama aishivyo BWANA, na bwana wangu mfalme aishivyo, hakika yake kila mahali atakapokuwapo mfalme, bwana wangu, ikiwa ni kwa kufa au ikiwa ni kwa kuishi, ndipo atakapokuwapo na mtumwa wako.
22 Basi Daudi akamwambia Itai, Haya, enenda ukavuke. Akavuka Itai, Mgiti na watu wake wote, na watoto wadogo wote waliokuwa pamoja naye.
23 Na nchi yote ikalia kwa sauti kuu, nao watu wote wakavuka, mfalme mwenyewe naye akavuka kile kijito Kidroni, na hao watu wote wakavuka, wakielekea njia ya nyika.
24 Na tazama, Sadoki naye akaja, na Walawi wote pamoja naye, huku wakilichukua sanduku la agano la Mungu; kisha wakalitua hilo sanduku la Mungu; Abiathari naye akapanda juu, hata watu wote walipokwisha kuutoka mji.
25 Naye mfalme akamwambia Sadoki, Rudisha sanduku la Mungu mjini; nikipata kibali machoni pa BWANA atanirudisha, na kunionyesha tena sanduku hili, na maskani yake;
26 lakini akisema kama hivi, Mimi si radhi nawe kabisa; basi, mimi hapa, na anitendee kama aonavyo kuwa vyema.