11 Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe.
12 Hivyo tutamfikia mahali po pote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye.
13 Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake.
14 Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana BWANA alikuwa amekusudia kulivunja shauri jema la Ahithofeli, ili BWANA alete mabaya juu ya Absalomu.
15 Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha.
16 Basi sasa pelekeni habari upesi kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye.
17 Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; nao huenda kumwambia mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini.