13 Na tena, kama ningaliitendea roho yake kwa hila; (wala hapana neno lo lote liwezalo kufichwa mbele ya mfalme); ndipo wewe mwenyewe ungalijitenga.
14 Ndipo Yoabu akasema, Siwezi kungoja na kusema nawe hivi. Akachukua vyemba vitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu moyoni, alipokuwa akali hai katikati ya ule mwaloni.
15 Kisha vijana kumi, waliomchukulia Yoabu silaha zake wakamzunguka, wakampiga Absalomu, na kumwua.
16 Kisha Yoabu akapiga tarumbeta, wakarudi watu toka kuwafuatia Israeli; kwani Yoabu akawazuia watu.
17 Nao wakamtwaa Absalomu wakamtupa katika shimo kubwa mle msituni, wakaweka juu yake chungu kubwa sana la mawe; kisha Israeli wote wakakimbia kila mtu hemani mwake.
18 Huyo Absalomu alipokuwa yu hai alikuwa ameitwaa na kujiinulia ile nguzo iliyoko bondeni mwa mfalme; kwa maana alisema, Mimi sina mtoto wa kulikumbusha jina langu; akaiita hiyo nguzo kwa jina lake mwenyewe nayo inaitwa ziara la Absalomu hata hivi leo.
19 Basi Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akasema, Niende mbio sasa, nikampelekee mfalme habari, jinsi BWANA alivyomlipiza kisasi juu ya adui zake.