1 Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.
2 Ndipo mfalme akawaita Wagibeoni akawaambia; (basi Wagibeoni si wa wana wa Israeli, ila ni wa masalio ya Waamori; na wana wa Israeli walikuwa wamewaapia; lakini Sauli akatafuta kuwaua katika juhudi yake kwa ajili ya wana wa Israeli na Yuda;)
3 basi Daudi akawaambia hao Wagibeoni, Niwatendee nini? Na kwa tendo gani nifanye upatanisho, mpate kuubariki urithi wa BWANA?
4 Na hao Wagibeoni wakamwambia, Si jambo la fedha wala dhahabu lililo kati ya sisi na Sauli, au nyumba yake; wala si juu yetu kumwua mtu ye yote katika Israeli. Akasema Mtakayoyanena, ndiyo nitakayowatendea ninyi.
5 Wakamwambia mfalme, Yule mtu aliyetupoteza, na kutufanyia shauri la kutuharibu, tusikae katika mipaka yo yote ya Israeli,
6 basi, na tutolewe watu saba katika wanawe, nasi tutawatundika mbele za BWANA katika Gibeoni, katika mlima wa BWANA. Mfalme akasema, Nitawatoa.
7 Lakini mfalme akamwachilia Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa ajili ya kiapo cha BWANA kilichokuwa kati yao, yaani, kati ya Daudi na Yonathani, mwana wa Sauli.