15 Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.
16 BWANA akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja.
17 Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unionyeshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami.
18 Tafadhali, usiondoke hapa hata nikujie, nikatoe zawadi yangu, na kuiweka mbele zako. Akasema, Nitangoja hata utakaporudi.
19 Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa.
20 Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo.
21 Ndipo malaika wa BWANA akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa BWANA akaondoka mbele ya macho yake.