20 Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo.
21 Ndipo malaika wa BWANA akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa BWANA akaondoka mbele ya macho yake.
22 Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa BWANA; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona BWANA uso kwa uso.
23 BWANA akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa.
24 Ndipo Gideoni akamjengea BWANA madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri.
25 Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Mtwae ng’ombe wa baba yako, yaani ng’ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo;
26 ukamjengee BWANA, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng’ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata.