31 Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake.
32 Basi akamwita Yerubaali siku hiyo, akisema, Baali na atete naye kwa ajili ya nafsi yake, kwa sababu ameibomoa madhabahu yake.
33 Wakati huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli.
34 Lakini roho ya BWANA ikaja juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata.
35 Kisha akatuma wajumbe waende kati ya Manase yote; wao nao walikutana pamoja ili kumfuata; kisha akatuma wajumbe waende kwa Asheri, na kwa Zabuloni, na kwa Naftali; nao wakakwea ili kumlaki.
36 Gideoni akamwambia Mungu, Ikiwa wewe utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema,
37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo katika kiwanja cha kupuria; na kama ukiwapo umande juu ya ngozi tu, na nchi yote ikiwa kavu, basi, hapo ndipo nitakapojua ya kuwa utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.