28 Hivyo Midiani walishindwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arobaini katika siku za Gideoni.
29 Kisha huyo Yerubaali, mwana wa Yoashi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe.
30 Gideoni alikuwa na wana sabini waliozawa na mwili wake; kwa maana alikuwa na wake wengi.
31 Na suria yake aliyekuwako Shekemu, yeye naye akamzalia mwana, naye akamwita jina lake Abimeleki.
32 Basi Gideoni mwana wa Yoashi akafa mwenye umri wa uzee mwema, akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake, katika Ofra ya Waabiezeri.
33 Kisha ikawa, mara alipokufa Gideoni, wana wa Israeli wakakengeuka tena, wakawaandama Mabaali kwa ukahaba, wakamfanya Baal-berithi kuwa ni mungu wao.
34 Kwani wana wa Israeli hawakumkumbuka BWANA, Mungu wao, ambaye ndiye aliyewaokoa na mikono ya adui zao wote pande zote;