6 mwili wake pia ulikuwa kama zabarajadi safi, na uso wake mfano wa umeme, na macho yake kama taa za moto, na mikono yake na miguu yake rangi yake kama shaba iliyosuguliwa sana, na sauti ya maneno yake kama sauti ya umati wa watu.
7 Nami, Danieli, nikaona maono haya peke yangu; maana wale watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona maono haya; lakini tetemeko kuu liliwashika, hata wakakimbia ili kujificha.
8 Basi nikaachwa peke yangu, nikaona maono haya makubwa, wala hazikubaki nguvu ndani yangu; maana uzuri wangu uligeuzwa ndani yangu kuwa uharibifu, wala sikusaziwa nguvu.
9 Walakini naliisikia sauti ya maneno yake; nami niliposikia sauti ya maneno yake, ndipo nikashikwa na usingizi mzito, na uso wangu umeielekea nchi.
10 Na tazama, mkono ukanigusa, ukaniweka juu ya magoti yangu, na vitanga vya mikono yangu.
11 Akaniambia, Ee Danieli, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima; maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia neno hili, nalisimama nikitetemeka.
12 Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako.