27 Danieli akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu;
28 lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho.Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi;
29 Wewe, Ee mfalme, mawazo yako yaliingia moyoni mwako kitandani pako ya mambo yatakayokuwa halafu; na yeye afunuaye siri amekujulisha mambo yatakayokuwa.
30 Lakini mimi, sikufunuliwa siri hii kwa sababu ya hekima iwayo yote niliyo nayo zaidi ya watu wengine walio hai, bali kusudi mfalme afunuliwe ile tafsiri, nawe upate kujua mawazo ya moyo wako.
31 Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha.
32 Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba;
33 miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo.