10 Mtaanguka kwa upanga; nitawahukumu katika mpaka wa Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
11 Mji huu hautakuwa sufuria lenu, wala ninyi hamtakuwa nyama ndani yake; nitawahukumu katika mpaka wa Israeli;
12 nanyi mtajua ya kuwa mimi ni BWANA; kwa maana hamuendi katika amri zangu, wala hamkuzishika hukumu zangu, bali mmetenda mambo kama hukumu za mataifa wanaowazunguka.
13 Ikawa, nilipotoa unabii, Pelatia, mwana wa Benaya, akafa. Ndipo nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kuu, nikasema, Ee Bwana MUNGU, je! Utawakomesha kabisa mabaki ya Israeli?
14 Neno la BWANA likanijia, kusema,
15 Mwanadamu, ndugu zako, naam, ndugu zako, watu wa jamaa zako, na nyumba yote ya Israeli, wote pia, ndio hao ambao wenyeji wa Yerusalemu wamewaambia, Jitengeni mbali na BWANA, nchi hii tumepewa sisi, iwe milki yetu;
16 basi nena, Bwana MUNGU asema hivi, Ikiwa mimi nimewahamisha, wakae katika mataifa, na ikiwa mimi nimewatawanya katika nchi kadha wa kadha, pamoja na hayo nitakuwa patakatifu kwao kwa muda mchache, katika nchi zile walizozifikilia.