6 Mmewaongeza watu wenu waliouawa ndani ya mji wenu, nanyi mmezijaza njia kuu zake waliouawa.
7 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Watu wenu waliouawa, ambao mmewalaza katikati yake, hao ndio nyama hiyo, na mji huu ndio sufuria; lakini ninyi mtatolewa nje kutoka katikati yake.
8 Ninyi mmeuogopa upanga; nami nitauleta upanga juu yenu, asema Bwana MUNGU.
9 Nami nitawatoa ninyi nje kutoka katikati yake, na kuwatia katika mikono ya wageni, nami nitafanya hukumu kati yenu.
10 Mtaanguka kwa upanga; nitawahukumu katika mpaka wa Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
11 Mji huu hautakuwa sufuria lenu, wala ninyi hamtakuwa nyama ndani yake; nitawahukumu katika mpaka wa Israeli;
12 nanyi mtajua ya kuwa mimi ni BWANA; kwa maana hamuendi katika amri zangu, wala hamkuzishika hukumu zangu, bali mmetenda mambo kama hukumu za mataifa wanaowazunguka.