1 Ikawa katika mwaka wa saba, mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja ili kuuliza kwa BWANA, wakaketi mbele yangu.
2 Neno la BWANA likanijia, kusema,
3 Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mmekuja kuniuliza neno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi.
4 Je! Utawahukumu, mwanadamu, utawahukumu? Uwajulishe machukizo ya baba zao;
5 uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile nilipochagua Israeli, na kuwainulia wazao wa nyumba ya Yakobo mkono wangu, na kujidhihirisha kwao katika nchi ya Misri, hapo nilipowainulia mkono wangu, nikisema, Mimi ni BWANA, Mungu wenu;
6 katika siku ile naliwainulia mkono wangu, kuwatoa katika nchi ya Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyowapelelezea, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote;
7 nikawaambia, Kila mtu kwenu na atupilie mbali machukizo ya macho yake, wala msijitie unajisi kwa vinyago vya Misri, Mimi ni BWANA, Mungu wenu.