2 akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana.
3 Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe.
4 Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la BWANA.
5 Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi.
6 Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
7 Basi nikatoa unabii kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu; na tazama, tetemeko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe.
8 Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu yake, ngozi ikaifunika juu yake; lakini haikuwamo pumzi ndani yake.