6 Nanyi mtaiandika milki ya mji, upana wake elfu tano, na urefu wake ishirini na tano elfu, kandokando ya mahali palipotolewa, iwe sehemu takatifu; nayo itakuwa ya nyumba yote ya Israeli.
7 Na sehemu itakayokuwa ya mkuu itakuwa upande huu, na upande huu, wa toleo takatifu, na wa milki ya mji, kulikabili toleo takatifu, na kuikabili milki ya mji, upande wa magharibi kuelekea magharibi, na upande wa mashariki kuelekea mashariki; na kwa urefu wake sawasawa na sehemu mojawapo, toka mpaka wa magharibi hata mpaka wa mashariki.
8 Katika nchi hiyo itakuwa milki kwake katika Israeli; wala wakuu wangu hawatawaonea watu wangu tena kabisa; bali watawapa nyumba ya Israeli nchi hiyo, kwa kadiri ya makabila yao.
9 Bwana MUNGU asema hivi; Na iwatoshe ninyi, enyi wakuu wa Israeli; ondoeni dhuluma na unyang’anyi; fanyeni hukumu na haki; ondoeni kutoza kwa nguvu kwenu katika watu wangu, asema Bwana MUNGU.
10 Mtakuwa na mizani ya haki, na efa ya haki, na bathi ya haki.
11 Efa na bathi zitakuwa za kipimo kimoja; ili kwamba bathi ichukue sehemu ya kumi ya homeri, na efa sehemu ya kumi ya homeri; kipimo chake kitakuwa kwa kadiri ya cheo cha kawaida cha homeri.
12 Nayo shekeli itakuwa gera ishirini; shekeli tano zitakuwa shekeli tano, shekeli kumi zitakuwa kumi, na shekeli hamsini zitakuwa mane yenu.