7 Ajali yako imekujia, wewe ukaaye katika nchi hii; majira yamewadia, siku ile inakaribia; siku ya fujo, wala si ya shangwe milimani.
8 Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote.
9 Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.
10 Angalia, siku hiyo; angalia, inakuja; ajali yako imetokea; fimbo imechanua, kiburi kimechipuka.
11 Udhalimu umeinuka, ukawa fimbo ya uovu; hapana mtu atakayesalia miongoni mwao, wala katika jamii yao, wala kitu katika utajiri wao; wala hakutakuwa kutukuka kati yao.
12 Majira yamewadia, siku ile inakaribia; huyo anunuaye asifurahi, wala asihuzunike auzaye; maana ghadhabu imewapata wote jamii.
13 Kwa maana auzaye hatakirudia kilichouzwa, wajapokuwa wangali hai; kwa sababu maono haya yawahusu wote jamii; hapana mmoja atakayerudi; wala hapana mtu atakayejitia nguvu katika uovu wa maisha yake.