7 Wakapiga mbiu katika Yuda yote na Yerusalemu, ya kwamba wana wote wa uhamisho wakusanyike pamoja huko Yerusalemu;
8 na ya kwamba mtu awaye yote asiyekuja katika muda wa siku tatu, kwa shauri lile la wakuu na wazee, basi aondolewe mali zake zote, akatengwe yeye mwenyewe na mkutano wa uhamisho.
9 Ndipo wanaume wote wa Yuda na Benyamini wakakusanyika katika muda wa siku tatu; ulikuwa mwezi wa kenda, siku ya ishirini ya mwezi; na watu wote wakaketi katika uwanja mbele ya nyumba ya Mungu, wakitetemeka kwa sababu ya neno hilo, na kwa sababu ya mvua kubwa.
10 Kisha Ezra, kuhani, akasimama, akawaambia, Mmekosa, mmeoa wanawake wageni, kuiongeza hatia ya Israeli.
11 Sasa basi, ungameni mbele za BWANA, Mungu wa baba zenu, mkatende alipendalo; mkajitenge na watu wa nchi, tena na wanawake wageni.
12 Ndipo mkutano wote wakajibu, wakasema, kwa sauti kuu, Kama ulivyosema katika habari yetu, ndivyo vitupasavyo kutenda.
13 Lakini watu hawa ni wengi, tena ni wakati wa mvua nyingi, nasi hatuwezi kusimama nje, tena kazi hii si kazi ya siku moja, wala ya siku mbili; maana tumekosa sana katika jambo hili.