1 Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule.
2 Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.
3 Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?
4 Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri.
5 Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli.