1 Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia,
2 Nena na wana wa Israeli, kisha upokee kwao fimbo, fimbo moja kwa ajili ya nyumba ya kila baba, katika wakuu wao wote, kama nyumba za baba zao zilivyo, fimbo kumi na mbili; kisha andika jina la kila mtu katika fimbo yake.
3 Na katika fimbo ya Lawi utaliandika jina la Haruni; maana, itakuwa fimbo moja kwa kila kichwa cha nyumba za baba zao.
4 Nawe utaziweka katika hema ya kukutania mbele ya huo ushahidi, hapo nikutanapo pamoja nanyi.
5 Kisha itakuwa, mtu huyo nitakayemchagua, fimbo yake itachipuka; nami nitayakomesha kwangu manung’uniko ya wana wa Israeli, wanung’unikiayo juu yenu.
6 Basi Musa akawaambia wana wa Israeli, ndipo wakuu wao wote wakampa fimbo, fimbo moja kwa kila mkuu, kama nyumba za baba zao zilivyokuwa, fimbo kumi na mbili; na fimbo ya Haruni ilikuwa kati ya fimbo zao.
7 Kisha Musa akaziweka hizo fimbo mbele za BWANA katika hema ya kukutania.