1 Kisha wana wa Israeli, mkutano wote, wakaingia bara ya Sini, katika mwezi wa kwanza, watu wakakaa Kadeshi; Miriamu akafa huko, akazikwa huko.
2 Na hapo hapakuwa na maji kwa ule mkutano; wakajikusanya juu ya Musa na juu ya Haruni.
3 Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za BWANA!
4 Mbona mmewaleta kusanyiko la BWANA hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu?
5 Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa.
6 Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano, wakaenda hata mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa BWANA ukawatokea.