12 BWANA akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa.
13 Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na BWANA, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kati yao.
14 Kisha Musa akatuma wajumbe kutoka Kadeshi wamwendee mfalme wa Edomu, na kusema, Ndugu yako Israeli asema, Wewe wazijua taabu zote zilizotupata;
15 jinsi baba zetu walivyotelemkia Misri, nasi tulikaa Misri muda mwingi, nao Wamisri walitutenda vibaya sana, na baba zetu pia;
16 tena tulipomlilia BWANA, akatusikiza sauti yetu, akamtuma malaika, na kututoa tutoke Misri; nasi tupo hapa Kadeshi, mji wa mpakani mwako mwa mwisho;
17 tafadhali utupe ruhusa tupite katika nchi yako; hatutapita katika mashamba, wala katika mashamba ya mizabibu, wala hatutakunywa maji ya visimani; tutaifuata njia kuu ya mfalme, tusigeuke kwenda upande wa kuume, wala upande wa kushoto, hata tutakapopita mpaka wako.
18 Edomu akamwambia, Hutapita katika nchi yangu, nisije nikakutokea kupigana nawe kwa upanga.