18 Edomu akamwambia, Hutapita katika nchi yangu, nisije nikakutokea kupigana nawe kwa upanga.
19 Wana wa Israeli wakamwambia, Tutakwea kwa njia kuu; tena kama tukinywa maji yako, mimi na wanyama wangu wa mifugo, ndipo nitakulipa thamani yake; nipe ruhusa nipite kwa miguu yangu wala sitaki neno lingine lo lote.
20 Akamwambia, Hutapita katika nchi yangu. Kisha Edomu akamtokea ili kupigana naye, na watu wengi, na kwa mkono wa nguvu.
21 Basi hivyo Edomu akakataa kumpa Israeli ruhusa kupita katika mipaka yake; kwa hivyo Israeli akageuka na kumwacha.
22 Kisha wakasafiri kutoka Kadeshi; wana wa Israeli, mkutano mzima, wakafikilia mlima wa Hori.
23 BWANA akanena na Musa na Haruni katika mlima wa Hori, karibu na mpaka wa nchi ya Edomu, akawaambia,
24 Haruni atakusanywa awe pamoja na watu wake; kwa kuwa hataingia katika nchi niliyowapa wana wa Israeli, kwa sababu mliasi kinyume cha neno langu hapo penye maji ya Meriba.