6 Tena kama amekwisha kuolewa na mume, wakati huo wa nadhiri zake, au wa neno hilo alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia;
7 na mumewe akasikia, naye akamnyamazia siku hiyo aliyosikia neno hilo; ndipo nadhiri zake zitathibitika, na vile vifungo ambavyo ameifunga nafsi yake vitathibitika.
8 Lakini kama mumewe akimkataza siku hiyo aliyolisikia; ndipo ataitangua nadhiri yake iliyo juu yake na neno alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia; na BWANA atamsamehe
9 Lakini nadhiri ya mjane, au ya mwanamke aliyeachishwa mume, kila neno ambalo ameifunga nafsi yake kwalo, litathibitika juu yake.
10 Tena kama aliweka nadhiri nyumbani mwa mumewe, au kama aliifunga nafsi yake kwa kifungo pamoja na kiapo,
11 na mumewe alisikia akamnyamazia, wala hakumkataza; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichojifungia kitathibitika.
12 Lakini kama mumewe alizibatilisha na kuzitangua siku hiyo aliyozisikia, ndipo kila neno lililotoka midomoni mwake katika hizo nadhiri zake, au katika kile kifungo cha nafsi yake, halitathibitika; huyo mumewe amezitangua; na BWANA atamsamehe.