6 Siku hizo zote ambazo alijiweka awe wa BWANA asikaribie maiti.
7 Hatajitia unajisi kwa ajili ya baba yake, wala kwa ajili ya mamaye, wala kwa nduguye mume, wala kwa umbu lake, wakifa wao; kwa sababu ya huku kujiweka kwa Mungu ni juu ya kichwa chake.
8 Siku zote za kujitenga kwake, yeye ni mtakatifu kwa BWANA
9 Na kama mtu ye yote akifa ghafla karibu naye, akajitia unajisi kichwa cha kutengwa kwake, ndipo atakinyoa kichwa siku hiyo ya kutakaswa kwake, atakinyoa siku ya saba.
10 Tena siku ya nane ataleta hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, aende nao kwa kuhani, hata mlangoni pa hema ya kukutania;
11 naye kuhani atasongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, naye atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa sababu aliingia kosani kwa ajili ya mfu, naye atatakasa kichwa chake siku iyo hiyo.
12 Kisha ataziweka kwa BWANA hizo siku za kujitenga kwake, naye ataleta mwana-kondoo mume wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya hatia; lakini hizo siku za kwanza hazitahesabiwa, kwa kuwa kule kujitenga kwake kulitiwa unajisi.