20 Basi Musa na Haruni, na mkutano wote wa wana wa Israeli, wakawafanyia Walawi mambo hayo; kama hayo yote BWANA aliyomwagiza Musa kwa habari za hao Walawi, ndivyo wana wa Israeli walivyowafanyia.
21 Walawi wakajitakasa na dhambi, nao wakafua nguo zao; kisha Haruni akawasongeza mbele za BWANA wawe sadaka ya kutikiswa; Haruni akafanya kwa ajili yao ili kuwatakasa.
22 Kisha baada ya hayo Walawi wakaingia ili wafanye utumishi wao ndani ya hema ya kukutania mbele ya Haruni na mbele ya wanawe; kama BWANA alivyomwagiza Musa kwa habari za hao Walawi, ndivyo walivyowafanyia.
23 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
24 Mambo yawapasayo hao Walawi ni haya; tangu waliopata umri wa miaka ishirini na mitano na zaidi wataingia ndani ili watumike utumishi katika kazi ya hema ya kukutania;
25 tena tangu waliopata umri wa miaka hamsini wataacha kutumika huo utumishi, wasitumike tena;
26 lakini watatumika pamoja na ndugu zao katika hema ya kukutania, kushika ulinzi, lakini wasitumike katika huo utumishi tena. Ndivyo utakavyowafanyia Walawi katika mambo ya ulinzi wao.