6 BWANA, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, Mlivyokaa katika mlima huu vyatosha;
7 geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo Araba, na nchi ya vilima-vilima, na huko Shefela, na Negebu, na pwani-pwani, nchi ya Wakanaani, na Lebanoni, mpaka mto huo mkubwa, mto wa Frati.
8 Angalieni, nimewawekea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi BWANA aliyowaapia baba zenu, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao.
9 Nami wakati ule niliwaambia, nikasema, Siwezi mimi mwenyewe kuwachukua peke yangu.
10 BWANA, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi, nanyi, angalieni, mmekuwa leo mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi.
11 BWANA, Mungu wa baba zenu, na awafanye kuwa wengi mara elfu kuliko mlivyo, na kuwabarikia, kama alivyowaahidi.
12 Nitachukuaje peke yangu mimi mwenyewe udhia wenu, na mzigo wenu, na mateto yenu?